Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, mfululizo wa mada za Mahdawiyya wenye anwani “Kuielekea Jamii Bora”, kwa lengo la kueneza mafundisho na maarifa yanayohusiana na Imam wa Zama (aj), unawasilishwa kwenu enyi watu wa elimu na utambuzi.
Katika sehemu mbili zilizopita, tuliangalia kwa ufupi majukumu ya jumla na pia jukumu muhimu zaidi la wanawake katika kufanikisha malengo ya Mwenyezi Mungu na kuandaa mazingira ya kudhihiri Mwokozi wa wanadamu. Katika sehemu hii, tutajibu maswali mawili yanayohusiana na nafasi na hadhi ya wanawake katika kudhihiri na utawala wa Imam wa Zama (aj).
Je, miongoni mwa watu 313 ambao ni wasaidizi maalumu wa Imam Mahdi (aj), je! Wanawake pia watakuwepo?
Katika hadithi ndefu iliyopokewa na Jabir kutoka kwa Imam al-Baqir (as), imekuja:
"وَاللَّهِ ثَلاَثُمِائَةٍ وَ بِضْعَةَ عَشَرَ رَجُلاً فِیهِمْ خَمْسُونَ امْرَأَةً یَجْتَمِعُونَ بِمَکَّةَ عَلَی غَیْرِ مِیعَادٍ"
"Naapa kwa Mwenyezi Mungu! Watu mia tatu na zaidi ya kumi watakuja, na miongoni mwao wamo wanawake hamsini, watakusanyika Makka pasi na makubaliano ya awali."
(Tafsīr Ayyāshī, Juz. 1, uk. 65)
Jambo muhimu katika riwaya hii ni kwamba kuna tafsiri mbili kuhusu kauli “فِیهِمْ”: Tafsiri ya kwanza: wanawake 50 ni sehemu ya wale watu 313. Tafsiri ya pili: wanawake 50 watakuwepo pamoja na wanaume 313.
Jambo jingine kuhusu riwaya hii ni kwamba; imekuja katika Tafsīr Ayyāshī, na kwa kuwa riwaya zilizopokewa na Ayyashi nyingi ni mursal, hali hii imepunguza nguvu ya kitabu hicho.
(Hadithi mursal maana yake ni kwamba mlolongo wa wapokezi wa hadithi haukutajwa.)
Riwaya hiyo hiyo kwa sanad imetajwa pia katika kitabu cha Ghaybat an-Nu‘mānī, lakini bila sehemu ya: "فِیهِمْ خَمْسُونَ اِمْرَأَةً"
"فَیَجْمَعُ اللَّهُ عَلَیْهِ أَصْحَابَهُ ثَلَاثَمِائَةٍ وَ ثَلَاثَةَ عَشَرَ رَجُلًا وَ یَجْمَعُهُمُ اللَّهُ لَهُ عَلَی غَیْرِ مِیعَادٍ"
"Mwenyezi Mungu atawakusanya kwake masahaba wake mia tatu na kumi na watatu, na atawakusanya bila makubaliano ya awali."
(Ghaybat an-Nu‘mānī, uk. 282)
Pia katika kitabu Ikhtisās cha Sheikh Mufid, riwaya hiyo imekuja bila sehemu ya: "فِیهِمْ خَمْسُونَ اِمْرَأَةً"
"فَیَجْمَعُ اللَّهُ لَهُ أَصْحَابَهُ ثَلَاثَ مِائَةٍ وَ ثَلَاثَةَ عَشَرَ رَجُلًا فَیَجْمَعُهُمُ اللَّهُ لَهُ عَلَی غَیْرِ مِیعَادٍ"
"Mwenyezi Mungu atawakusanya kwake masahaba wake mia tatu na kumi na watatu, na atawakusanya bila makubaliano ya awali."
(Ikhtisās, uk. 255)
Jambo jingine muhimu ni kwamba; kwa kuzingatia dalili zilizopo, neno “rajul” katika riwaya hizi linaeleweka kuwa linamaanisha mwanaume, si mwanamke.
Kufananishwa kwa wasaidizi maalumu wa Imam wa Zama (aj) na watu wa Badr:
"یَجْمَعُ اَللَّهُ عَزَّ وَ جَلَّ لَهُ مِنْ أَقَاصِی اَلْبِلاَدِ عَلَی عَدَدِ أَهْلِ بَدْرٍ ثَلاَثَمِائَةٍ وَ ثَلاَثَةَ عَشَرَ رَجُلاً"
"Mwenyezi Mungu atawakusanya kutoka miji ya mbali watu mia tatu na kumi na tatu kwa idadi ya watu wa Badr."
(Kamāl ad-Dīn wa Tamām an-Ni‘mah, uk. 264)
Kufananishwa kwao na watu wa Talut (as):
"اَلْقَلِیلُ اَلَّذِینَ لَمْ یَشْرَبُوا وَ لَمْ یَغْتَرِفُوا ثَلَثَمِائَةٍ وَ ثَلَاثَةَ عَشَرَ رَجُلاً"
"Waliosalia wachache ambao hawakunywa maji walikuwa mia tatu na kumi na tatu."
(Tafsīr Nūr ath-Thaqalayn, Juz.1, uk.248)
Na ni wazi kwamba watu 313 katika vita vya Badr na katika jeshi la Talut dhidi ya Jalut wote walikuwa ni wanaume.
Kwa hiyo kwa mtazamo wa elimu ya hadithi, kuthibitisha uwepo wa wanawake miongoni mwa watu 313 au pamoja nao ni jambo lenye ugumu, kwa sababu hadithi moja tu ndiyo imeashiria jambo hilo na yenyewe ilikuwa mursal, ilhali zipo riwaya zenye sanad zinazowahusisha watu 313 kuwa wanaume pekee.
Lakini kutokana na yaliyotajwa katika sehemu mbili zilizopita na yale yatakayokuja baadaye, kutokuwepo kwa wanawake miongoni mwa watu 313 (kwa mujibu wa hoja zilizopo) hakumaanishi kabisa kudharauliwa kwa nafasi na hadhi ya mwanamke.
Kwa sababu kutakuwa na wasaidizi wengi katika makundi mbalimbali watakaojiunga na Imam wa Zama (as), na idadi yao haitahesabika. Hivyo wanawake katika kudhihiri na serikali ya Mahdi — kama ilivyotajwa hapo awali — watakuwa na nafasi na hadhi maalumu.
Je, miongoni mwa watu watakaorejea (Raj'a), wanawake pia watakuwepo?
Katika utafiti huu, hatuna nia ya kuchunguza hatua ambayo wanawake watarejea ndani yake, wala idadi yao halisi au majina yao kamili.
Jambo muhimu ni msingi wa suala la kurejea kwa wanawake; yaani kwamba katika historia wamekuwepo na wataendelea kuwepo wanawake ambao wamefikia viwango vya juu kabisa vya imani na maarifa, kiasi kwamba watapewa tawfiki ya kurejea duniani na kuandamana na Wasii wa mwisho wa Mwenyezi Mungu.
Imam Sadiq (as) amesema katika riwaya:
"یُکَرُّ مَعَ اَلْقَائِمِ (عَلَیْهِاَلسَّلاَمُ) ثَلاَثَ عَشْرَةَ اِمْرَأَةً. قُلْتُ: وَ مَا یَصْنَعُ بِهِنَّ؟ قَالَ: یُدَاوِینَ اَلْجَرْحَی، وَ یَقُمْنَ عَلَی اَلْمَرْضَی، کَمَا کَانَ مَعَ رَسُولِ اَللَّهِ (صَلَّی اَللَّهُ عَلَیْهِ وَ آلِهِ). قُلْتُ: فَسَمِّهِنَّ لِی. فَقَالَ: اَلْقِنْوَاءُ بِنْتُ رُشَیْدٍ، وَ أُمُّ أَیْمَنَ، وَ حَبَابَةُ اَلْوَالِبِیَّةُ، وَ سُمَیَّةُ أُمُّ عَمَّارِ بْنِ یَاسِرٍ، وَ زُبَیْدَةُ، وَ أُمُّ خَالِدٍ اَلْأَحْمَسِیَّةُ، وَ أُمُّ سَعِیدٍ اَلْحَنَفِیَّةُ، وَ صُبَانَةُ اَلْمَاشِطَةُ، وَ أُمُّ خَالِدٍ اَلْجُهَنِیَّةُ."
“Pamoja na al-Qa’im (as), wanawake kumi na watatu watarejea.”
Mpokezi anasema: Nikasema: “Watapewa jukumu gani?”
Akasema: “Watatibu majeruhi na kuwahudumia wagonjwa, kama walivyokuwa wakifanya pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww).”
Nikasema: “Tafadhali nitajie majina yao.”
Akasema: “Qanwaa binti Rushaid, Ummu Ayman, Hubabah al-Walibiyyah, Sumayyah mama wa Ammar bin Yasir, Zubaydah, Ummu Khalid al-Ahmasiyyah, Ummu Sa‘id al-Hanafiyyah, Subanah mtengeneza nywele, na Ummu Khalid al-Juhaniyyah.”
(Dalā'il al-Imāmah, Juz. 1, uk. 484)
Katika vitabu vingine pia, idadi na majina ya baadhi ya wanawake wengine watakaorejea imetajwa. (Kama ilivyoelezewa awali, majina yao, idadi yao na wakati wa kurejea kwao si mada ya utafiti wetu.)
Jambo muhimu ambalo linaweza kuwasaidia wanawake katika njia ya kushikamana na dini, kupata maarifa na kudumu katika dini ya Mwenyezi Mungu, ni kuzingatia sifa za wanawake waliotajwa katika riwaya hizi, ambazo tutazitaja baadhi yake.
Uhuru wa nafsi, umadhubuti na kusimama imara kukabiliana na safu ya batili, ni sifa kuu ya pamoja inayoweza kupatikana kwa wanawake watakaorejea.
Mtume mtukufu wa Uislamu (saww) amesema kuhusu Subanah, mtengeneza nywele wa binti wa Firauni:
“Nilipopelekwa Mi‘raj, ilinifikia harufu nzuri sana, nikamwambia Jibril: ‘Harufu hii ni ya nini?’ Akasema: ‘Hii ni harufu ya mtengeneza nywele wa familia ya Firauni na watoto wake.’ Alikuwa akimchana nywele binti wa Firauni, ghafla kichanuo kikaanguka kutoka mkononi mwake na akasema: Bismillah. Binti wa Firauni akamuuliza: ‘Je, unamkusudia baba yangu?’ Yule mwanamke akasema: ‘La, bali ninamkusudia Mola wangu, Mola wako, na Mola wa baba yako.’ Binti huyo akasema: ‘Hakika nitamwambia baba yangu.’ Yule mwanamke akasema: ‘Mwambie utakavyo.’ Binti huyo akamwambia baba yake jambo hilo. Firauni akamwita mwanamke yule pamoja na watoto wake na akamuuliza: ‘Mola wako ni nani?’ Yule mwanamke akasema: ‘Mola wangu na wako ni Mwenyezi Mungu.’
Firauni akaamuru tanuri la shaba litengenezwe na liwekwe moto mkali, kisha akaamuru mwanamke huyo na watoto wake waletwe. Yule mwwanamke alipofikishwa mbele ya tanuru akasema: ‘Nina ombi moja kwako.’ Firauni akasema: ‘Ni lipi?’
Akasema yule mwanamke: ‘Nataka mifupa yangu na mifupa ya watoto wangu uikusanye na kuizika.’
Firauni akasema: ‘Kwa sababu ya haki uliyonayo juu yetu (kwa huduma zako za zamani), nitakufanyia hilo.’Kisha akaamuru watoto wake watupwe mmoja baada ya mwingine ndani ya tanuri hadi akafikia mtoto wake wa mwisho aliyekuwa bado ananyonya. Mtoto huyo akasema: ‘Ewe mama yangu! Subiri na vumilia, kwa sababu wewe uko juu ya haki.’ Kisha yule mwanamke naye akatupwa ndani ya tanuri pamoja na mtoto wake.”
(Bihar al-Anwar, Juz. 13, uk. 163)
Kuhusu Sumayyah, mama wa Ammar, imepokewa:
"وَ کَانَتْ مِمَّنْ تُعَذَّبُ فِی اَللَّهِ لِتَرْجِعَ عَنْ دِینِهَا فَلَمْ تَفْعَلْ فَمَرَّ بِهَا أَبُو جَهْلٍ فَطَعَنَهَا فِی قَلْبِهَا فَمَاتَتْ"
“Na yeye (Sumayyah) alikuwa ni miongoni mwa wanaoteswa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ili waachane na dini yao, lakini hakufanya hivyo. Kisha Abu Jahl alipita karibu naye na akamchoma moyoni mwake, na akafariki.”
(Bihar al-Anwar, Juz.18, uk.241)
Na kuna mifano mingine mingi.
Tanbihi:
Mazingira na sababu za kijamii ni miongoni mwa visingizio ambavyo baadhi ya watu, hususan wanawake katika jamii, hutumia kuelezea udhaifu wa imani na maarifa yao.
Hali ya kuwa, kutafakari maisha ya wanawake waliobadilisha historia katika Uislamu kunaonesha kwamba; katika njia ya malengo ya Mwenyezi Mungu na kuelekea kwa Muumba, hakuna mtu wala kitu kinachoweza kumzuia mwanadamu.
Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Qur’ani Tukufu, anampotaja Bibi Asiya (as), hamtaji kwa jina lake, bali anamtaja kwa jina la: "امْرَأَتَ فِرْعَوْنَ" "Mke wa Firauni" ili kuwafahamisha wanaume na wanawake waumini wote kwamba; yeye aliishi ndani ya kasri la dhalimu wa zama zake, na huku akiwa hana msaidizi yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu, aliweza kuwa mfano kwa watu wote.
Neno la mwisho ni kwamba; Raj'a si jambo linalowahusu waliopita tu, bali pia linawahusu watakaokuja baadaye.
Ndiyo maana tumesisitiziwa kusoma Dua ya Ahdi:
«اللَّهُمَّ إِنْ حَالَ بَینِی وَ بَینَهُ الْمَوْتُ الَّذِی جَعَلْتَهُ عَلَی عِبَادِک حَتْما مَقْضِیا، فَأَخْرِجْنِی مِنْ قَبْرِی مُؤْتَزِرا کفَنِی شَاهِرا سَیفِی مُجَرِّدا قَنَاتِی مُلَبِّیا دَعْوَةَ الدَّاعِی فِی الْحَاضِرِ وَ الْبَادِی.»
“Ewe Mwenyezi Mungu! Ikiwa kifo ambacho umekiweka kuwa ni hukumu isiyoweza kuepukika juu ya waja wako kitakuwa kimenitenganisha naye, basi nitoe kutoka kaburini mwangu nikiwa nimevaa sanda yangu, nikiwa nimeutoa upanga wangu, nikiwa nimeinua mkuki wangu, nikiwa ninaitikia wito wa mlinganaji katika miji na majangwani.”
Na bila shaka, ili kufikia lengo hili lenye kuvutia na kupendeza, ni lazima tujipambe kwa sifa zile ambazo zimetajwa katika riwaya kuhusu wale watakaorejea (Raj'a); na katika njia hii hakuna tofauti yoyote kati ya mwanamume na mwanamke.
ــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــــ
1.
«لَمَّا أُسْرِیَ بِی مَرَّتْ بِی رَائِحَةٌ طَیِّبَةٌ فَقُلْتُ لِجَبْرَئِیلَ مَا هَذِهِ اَلرَّائِحَةُ قَالَ هَذِهِ مَاشِطَةُ آلِ فِرْعَوْنَ وَ أَوْلاَدُهَا کَانَتْ تَمْشُطُهَا فَوَقَعَتِ اَلْمُشْطَةُ مِنْ یَدِهَا فَقَالَتْ بِسْمِ اَللَّهِ فَقَالَتْ بِنْتُ فِرْعَوْنَ أَبِی فَقَالَتْ لاَ بَلْ رَبِّی وَ رَبُّکِ وَ رَبُّ أَبِیکِ فَقَالَتْ لَأُخْبِرَنَّ بِذَلِکِ أَبِی فَقَالَتْ نَعَمْ فَأَخْبَرَتْهُ فَدَعَا بِهَا وَ بِوُلْدِهَا وَ قَالَ مَنْ رَبُّکِ فَقَالَتْ إِنَّ رَبِّی وَ رَبُّکَ اَللَّهُ فَأَمَرَ بِتَنُّورٍ مِنْ نُحَاسٍ فَأُحْمِیَ فَدَعَا بِهَا وَ بِوُلْدِهَا فَقَالَتْ إِنَّ لِی إِلَیْکَ حَاجَةً قَالَ وَ مَا هِیَ قَالَتْ تَجْمَعُ عِظَامِی وَ عِظَامَ وُلْدِی فَتَدْفَنُهَا قَالَ ذَاکِ لَکِ لِمَا لَکِ عَلَیْنَا مِنْ حَقٍّ فَأَمَرَ بِأَوْلاَدِهَا فَأُلْقُوا وَاحِداً وَاحِداً فِی اَلتَّنُّورِ حَتَّی کَانَ آخِرُ وُلْدِهَا وَ کَانَ صَبِیّاً مُرْضَعاً فَقَالَ اِصْبِرِی یَا أُمَّاهْ إِنَّکِ عَلَی اَلْحَقِّ فَأُلْقِیَتْ فِی اَلتَّنُّورِ مَعَ وُلْدِهَا.»
Maoni yako